Habari hii na BBC Swahili
Msanii
wa kike wa filamu Tanzania Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama
Lulu,amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya msanii
mwingine wa filamu Marehemu Steven Kanumba.
Amefikishwa
mahakamani ikiwa ni siku nne, tangu alipokamatwa mara baada ya kifo cha
msanii huyo ambaye inaaminika kuwa walikuwa na uhusiano wa Kimapenzi.
Mbele
ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam,Bi
Augustina Mbando,Elizabeth Michael Kimemeta ajulikanaye kama Lulu kwa
jina la Usanii,aliwasili mahakamani hapo akiwa chini ya Ulinzi mkali wa
askari Polisi waliokuwa wamevaa kiraia na wengine wakiwa wamejihami kwa
silaha.
Mara
baada ya Kufikishwa mahakamani,upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili
wa serikali Bi Elizabeth Kaganda ulimsomea shtaka moja ambalo ni la
mauaji, kosa ambalo ni kinyume cha sheria ya kanuni ya adhabu kifungu
cha 196.
Wakili
huyo wa serikali Bi Elizabeth Kaganda,alidai mbele ya mahakama kuwa
mnamo tarehe 07 mwezi April mwaka 2012,katika eneo la Sinza
Vatican,msanii Elizabeth alimuua msanii Steven Kanumba.
Akiwa
amevalia gauni kubwa lijulikanalo kama dera lenye rangi ya Njano
mtandio wa rangi ya waridi na kandambili nyekundu mshtakiwa alionekana
kutokuwa na wasi wasi pamoja uzito wa tuhuma za mauaji anayokabiliwa
nayo huku akijibu maswali kadhaa kuhusu wasifu wake.
Msanii huyo alikanusha kuwa na umri wa miaka 18 baada
kuulizwa
,ambapo yeye amesisitiza kuwa ana umri wa miaka 17, hii ikiwa ni
tofauti na habari ambazo zimekuwa zikiripotiwa kuhusu umri wa msanii
huyo ambaye sasa anatambulika kama mshtakiwa.
Kesi hii ya mauaji inatajwa kwa mara ya kwanza na mshtakiwa hakutakiwa kukiri wala kukana mashtaka.
Upande wa mashtaka umeieleza mahakama kuwa kesi bado iko kwenye upelelezi ambapo inatarajiwa kutajwa tena April 23 mwaka huu.
Mshtakiwa amepelekwa rumande hadi siku hiyo wakati kesi hii itakapotajwa tena.
Kwa
upande mwingine tukio la kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo
kumefanywa kwa usiri mkubwa na kufanya waandishi wa habari wengi
wameshindwa kufuatilia kwa karibu tukio lenyewe.
Kufikishwa
mahakamani kwa msanii huyo na kusomewa shtaka la mauaji ya Kanumba
kumetokea siku moja baada na Marehemu Steven Kanumba kuzikwa katika
makaburi ya Kinondoni.
Mazishi
yake yalichukua sura ya kitaifa kutokana na umaarufu aliojijengea msani
huyo katika jamii ya watanzania na hata nchi za nje.